Kesha la Asubuhi Agosti 6- 12,2016

Agosti 6

Tunasafishwa kwa Damu ya Kristo

Damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.
I Yohanal:7.
              Kuhusu wakati wa Wayahudi, baadhi ya watu wanasema kilikuwa kipindi ambacho hakikuwa na hali ya kuwepo kwa Kristo , hakikuwa na rehema au neema. Kwa watu kama hao maneno Kristo aliyosema kwa Masadukayo yanawafaa, “hamyajui maandiko wala
uweza wa Mungu.” Wakati wa utamaduni wa Kiyahudi ulikuwa ni wakati wa udhihirisho wa ajabu wa uweza wa Mungu. Dhihirisho la kuwepo kwake lilikuwa la utukufu kiasi ambacho mwanadamu anayekufa asingeweza kustahimili. Musa, ambaye Mungu alimpenda sana, alisema, “Nimeshikwa na hofu na kutetemeka.” Lakini Mungu alimtia nguvu akaweza kustahimili utukufu huu wa ajabu na kufanya uso wa Musa kuakisi utukufu huu kutoka miimani kiasi kwamba watu hawakuweza kudumu kuutazama...
               Mfumo halisi wa kafara ulipangwa na Kristo na Adamu akapewa kama kielelezo kinachoonesha Mwokozi anayekuja, ambaye angebeba dhambi za ulimwengu na kufa iii kuukomboa. Kupitia kwa Musa, Kristo alitoa maelekezo dhahiri kwa wana wa Israeli
kuhusu sadaka za kafara... Ni wanyama wale tu waliokuwa safi na wenye thamani, ambao wangemwakilisha Kristo kwa ubora zaidi ,ndio waliokubalika kama sadaka kwa Mungu...
               Wana wa Israeli walikatazwa kula mafuta au damu... Sheria hii haikuhusu wanyama wa sadaka tu, bali pia ng’ombe wote waliotumika kwa chakula. Sheria hii ilikuwa imekusudiwa kusisitiza ndani yao ukweli wa muhimu kwamba kama isingekuwa dhambi kusingekuwa na umwagaji wa damu...
                Damu ya Mwana wa Mungu iliwakilishwa na damu ya mnyama aliyechinjwa na Mungu alikuwa amewekeza dhana zilizo dhahiri na wazi zilizobainisha kati ya vitakatifu na vya kawaida. Damu ilikuwa takatifu, kwa namna ambayo kupitia kumwagika kwa damu
ya Mwana wa Mungu pekee ndiko kungeleta upatanisho kwa ajili ya dhambi. Vilevile damu ilitumika kusafisha hekalu kutokana na dhambi za watu, kwa namna hiyo kuonesha kielelezo cha damu ya Kristo ambayo ndiyo pekee iwezayo kutakasa toka katika dhambi.






  
Agosti 7

Upatanisho Kupitia kwa Damu ya Kristo
Wala si hivyo tu, ita pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea hua upatanisho. Warumi 5:11.

              Mungu ashukuriwe kwamba yeye aliyemwaga damu yake kwa ajili yetu, yu hai kuitetea, anaishi akifanya upatanisho kwa ajili ya kila nafsi inayompokea yeye. “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” Damu ya Yesu Kristo inatutakasa kutoka katika dhambi zote...
Inatupasa kudumisha mbele yetu uelewa wa umuhimu wa damu ya Yesu. Ile damu inayotakasa maisha, damu inayodumisha uhai, inayokuja kutokana na imani iliyo hai, ndilo tumaini letu. Inatupasa tukue katika hali ya kutambua thamani yake isiyopimika, kwani inadumu kunena kwa ajili yetu pale tu ambapo kwa imani tunadai sifa yake stahilifu , huku tukitunza dhamiri yetu katika usafi na amani na Mungu. Hili linawakilishwa kama damu inayosamehe, ambayo imeunganika moja kwa moja na ufufuo na uzima wa Mkombozi wetu, ambayo kielelezo chake ni chemchemi inayotiririka bila kukoma kutoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu, maji ya mto wa uzima.
           Ishara ya ajabu ya ndege aliye hai ambaye huchovywa kwenye damu ya ndege aliyechinjwa na kisha kuwekwa huru aendelee na maisha ya raha [Walawi 14:4-81, kwetu sisi ni ishara ya upatanisho. Hapa mauti na uzima vilipatanishwa, vikiwasilisha kwa mwenye kuutafuta ukweli na hazina iliyofichwa, muunganiko wa damu inayosamehe na ufufuo na uzima wa Mkombozi wetu. Ndege aliyechinjwa alikuwa juu ya maji yenye uzima; ile chemchemi iliyokuwa ikitiririka ilikuwa ishara ya umuhimu usiokoma kutiririka, usiokoma kutakasa wa damu ya Kristo, Mwanakondoo aliyechinjwa tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu ...
            Yatupasa kuwa huru kuifikia damu ya upatanisho ya Kristo. Ni lazima tulione hili kama fursa ya thamani sana, baraka ya juu zaidi ,ambayo imepata kutolewa kwa mwanadamu mwenye dhambi ... Hii chemchemi ina kina kirefu sana na upana mkubwa sana na inaendelea kudumu kuliko maelezo! Kwa kila nafsi yenye kiu ya utakatifu kuna utulivu, kuna pumziko, kuna mvuto wenye kuhuisha wa Roho Mtakatifu na kisha mwendo mtakatifu, wa furaha, wenye amani na ushirika pamoja na Kristo.








Agosti 8

Tunahesabiwa Haki kwa Damu ya Kristo

Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Warumi 5:8,9.

            Kristo amefanya upatanisho kwa ajili ya dhambi, tena amebeba fedheha yake yote, dhihaka na adhabu; na licha ya hivyo, huku akiibeba dhambi, ameleta haki ya milele, iii muumini apate kuwa bila waa mbele za Mungu...
            Lakini wapo wengi wanaodai kuwa watoto wa Mungu ambao  wamewekeza katika kutumainia sehemu zingine, badala ya kwenye damu ya Kristo pekee. Wanapoombwa sana kuweka imani yao kikamilifu kwa Kristo kama Mwokozi aliye kamili, wengi
wanadhihirisha ukweli kwamba wana imani katika kile wanachofikiria kuwa wanaweza kufanya. Hawa husema, “Ninayo mengi sana ya kufanya kabla sijafaa kuja kwa Kristo.” Mwingine husema, “Nitakapokuwa nimetenda kwa kadiri niwezavyo yote niwezayo kutenda, ndipo Bwana Yesu atakuja kunisaidia.” Wanafikiria kwamba wanayo kazi kubwa sana ya kufanya wao wenyewe kuokoa roho zao wenyewe na kwamba Yesu ataingia na kukifanyia kazi kile kipande kinachopungua na kufanya kazi ya kumalizia kwa ajili ya wokovu wao. Maskini watu hawa, hawatakuwa na nguvu ndani yake Mungu hadi watakapomkubali Kristo kama Mwokozi kamili. Hawawezi kuongeza chochote kwa ajili ya wokovu wao.
          Wana wa Israeli walitakiwa kunyunyizia miimo ya milango yao damu ya mwanakondoo aliyechinjwa, ili wakati malaika wa mauti akipita kwenye nchi, wapate kuepuka uangamivu. Lakini ikiwa badala ya kufanya kitendo hiki sahili cha imani na utii, wangezuia miango na kuchukua tahadhari zote katika kumzuilia mbali malaika Mwangamizaji ,taabu zao zingekuwa za bure... Damu ilipoonekana kwenye miimo ya milango, ilitosha. Wokovu wa nyumba ulithibitishwa. Hivyo ndivyo ilivyo kazi ya wokovu; ni damu ya Yesu Kristo inayotutakasa kutoka katika dhambi zote.
            Kupitia ustahili wa damu yake, unaweza kushinda kila adui wa kiroho na kuponya kila udhaifu wa tabia.






Agosti 9

Wana wa Mungu kwa Njia ya Damu ya Kristo

Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake. Waebrania 10:19, 20.
             Kristo aliwambwa msalabani kati ya saa tatu na saa sita. Alikufa adhuhuri. Hii ilikuwa saa ya kafara ya jioni. Kisha pazia la hekalu, ambalo lilifunika utukufu wa Mungu ili kusanyiko la Israeli wasiuone, lilipasuka vipande viwili kutoka juu hadi chini.
             Kupitia kwa Kristo, utukufu wa patakatifu pa patakatifu uliokuwa umefichwa, ilipasa sasa udhihirishwe. Alikuwa ameuawa kwa ajili ya kila mtu na kwa njia ya sadaka hii, wana wa binadamu walikuwa wawe wana wa Mungu. Kwa namna iliyo wazi kabisa, utukufu wa Bwana ukionekana kama katika kioo, wanaomwamini Kristo walikuwa wabadilishwe na kufanana naye, kutoka utukufu hadi utukufu. Kiti cha rehema, ambapo utukufu wa Mungu ulikuwa katika patakatifu mno, kimefunguliwa wazi kwa wale wote wanaomkubali Kristo kama kipatanishi kwa ajili ya dhambi na kupitia njia hii, wanaletwa katika ushirika na Mungu. Pazia limepasuliwa, kuta za utengano zimevunjwa, maandiko ya zile sherehe yameondolewa. Kutokana na sifa stahilifu za damu yake, adui amekomeshwa.
  Kisa rahisi cha msalaba wa Kristo, mateso na kufa kwake kwa ajili ya ulimwengu, ufufuo na kupaa kwake, upatanisho wake kwa niaba ya mwenye dhambi mbele za Baba, kisa hiki kitaudhili na kuuvunja moyo wenye dhambi ulio mgumu na kumleta mwenye dhambi katika toba. Roho Mtakatifu ataliweka jambo hili mbele zake katika mwonekano mpya, mwenye dhambi naye atatambua kwamba dhambi ni uovu mkubwa kiasi hicho cha kugharimu kafara kubwa hivyo ili kufanya upatanisho kwa sababu yake... Dhambi, lazima iwe ni ya kutisha kiasi kwamba hakuna tiba pungufu ya kifo cha Mwana wa Mungu ambayo ingeweza kumwokoa mwanadamu kutokana na matokeo ya hatia. Kwa nini hili lilifanywa kwa niaba ya mwanadamu? — Ni kwa sababu Mungu alimpenda na hakuwa tayari yeyote apotee, lakini kwamba wote wafikilie toba, mwamini Yesu kama Mwokozi wako binafsi na uwe na uzima wa milele.





Agosti 10

Kifo cha Kristo Kinatupatanisha na Mungu

Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Warumi 5:10.

                Msalaba umepewa uwezo ambao hakuna lugha iwezayo kuuelezea. Kafara ya Kristo kwa niaba ya wanadamu inaaibisha jitihada zetu dhaifu na mbinu zetu za kuufikia na kuuinua ubinadamu, kusaidia wanaume na wanawake wenye dhambi wamwone Yesu.
                Lazima kazi ya wana na binti za Mungu iwe ya ama tofauti na yoyote ambayo imepata kudhihirishwa kwa watu wengi. Kama wanampenda Yesu, watakuwa na mawazo mapana ya upendo ambao umeoneshwa kwa mwanadamu aliyeanguka dhambini, upendo ambao ulihitaji kutolewa kwa sadaka aghali kiasi hicho ili kumwokoa mwanadamu. Mwokozi wetu anahitaji ushirikiano wa kila mwana na binti wa Adamu ambaye amekuwa mwana na binti wa Mungu... Mwokozi wetu alitamka kuwa alileta kutoka mbinguni uzima wa milele kama msaada. Ilimpasa ainuliwe juu kwenye msalaba wa Kalvari ili avute watu wote kwake. Tutawezaje basi kununua urithi wa Kristo? Yapasa waoneshwe wema, shukrani,  upole, huruma na upendo. Kisha tutaweza kufanya kazi na kubarikiana sisi kwa sisi. Katika kazi hii tuna zaidi ya undugu wa kibinadamu. Tuna ushirika wenye utukufu wa malaika wa kimbingu. Hawa huwa wanashirikiana nasi katika kazi ya kuelimisha katika viwango vya juu na vya chini.
                  Akiwa ameingia katika kazi hii, kazi ya ajabu kwa ajili ya ukombozi wetu, Kristo aliazimia akishirikiana na Baba yake kutozuia. chochote, hata kiwe na gharama kubwa kiasi gani,kutozuia chochote hata kiwe kimekadiriwa kuwa juu kiasi gani, ambacho kingeokoa mwenye dhambi dhaifu. Angeweza kutoa mbingu yote kwa ajili ya kazi hii ya wokovu, ya kurejesha sura ya kimaadili ya Mungu kwa mwanadamu... Kuwa mtoto wa Mungu ni kuwa wamoja na Kristo katika Mungu na kutoa mikono yetu katika upendo wa dhati, wenye kujitoa nafsi iii kuimarisha na kubariki roho zinazoangamia katika dhambi zao.





Agosti 11

Kristo Ametukomboa Kutoka Kwenye Mauti ya Milele

Aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye

tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa 2Wakorintho 1:10.

                 Mwokozi wetu alikuja hapa duniani iii apate kustahimili katika mwili wa kibinadamu majaribu yote yanayomsumbua mwanadamu. Katika maisha yake alizipima nguvu za adui mkuu anazotumia kudanganya, kuvuta na kuangamiza. Akiwa Mkombozi wa watu, anaonya binadamu dhidi ya kutafuta mambo yale mengine ambayo yataondoa mtu kutoka kwenye njia nyembamba. Ameweka njia tukufu kwa ajili ya wale wanaosafiri kwenda kwenye makao ya mbinguni ambapo amekwenda kuandaa kwa ajili ya wote ambao watajiandaa wenyewe kuwa washirika wa familia ya kifalme...
                  Kwa njia ya maisha yake, Kristo alimnunua kila binadamu. Alikufa kifo cha kikatili ili kuokoa binadamu toka kwenye mauti ya milele.Alitoa maisha yake yasiyo na dhambi iii apate kwa ajili ya wenye dhambi maisha ambayo yanalingana na maisha ya Mungu. Kupitia kifo chake, alitoa njia ambayo kwa hiyo, mwanadamu anaweza kuvunja
uhusiano na Shetani, kurejea kwenye utii wake kwa Mungu na kwa njia ya imani kwa Mkombozi kupata msamaha...
                  Yeye aliye na uwezo mbinguni na duniani anao uwezo wa kurejeza kila roho inayotubu, inayoamini. Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu. Yeye anapendezwa na kila mtu, kwani alilipa bei ya uhai wake mwenyewe ili asiwepo yeyote atakayepotea milele.
                     Watumishi wa Kristo wanaweza na sharti waweze kukutana na kushinda kila jaribu. Yapasa waseme, “Mimi sio wangu mwenyewe; nimenunuliwa kwa gharama. Kwa kafara isiyo na kikomo ambayo Kristo ameifanya kwa ajili yangu, amefanya lisiwe katika uwezo wangu kumpatia yeye zaidi ya kile anachohitaji. Vyote ni vyake. Ameninunua, mwili, nafsi na roho. Anahitaji muda wangu wote, uwezo wangu wote.”
                      Wale wanaompokea na kumwamini yeye wanakuwa watoto wa Mungu kiroho. Wanakuwa wamefanywa kuwa sehemu ya familia ya kifalme na kadiri wanavyojitahidi kufanya mapenzi ya Mungu, wanafanana na sura yake.




Agosti 12

Inatupasa Kuonea Fahari Msalaba Tu

Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.
Wagalatia6:14.

              Msalaba wa Kristo, -- ni wangapi wanaoamini kuwa ndivyo ulivyo? Ni wangapi wanaoufanya kuwa kiini cha majifunzo yao na kujua umuhimu wake wa kweli? Kusingekuwa na Mkristo katika dunia yetu bila ya msalaba wa Kristo... Geuka toka kwenye mifano ya dunia, ukome kutoka katika kutukuza watu wanaofikiriwa kuwa wakuu; geuza akili kutoka katika utukufu wa kila kitu kingine isipokuwa msalaba Wa Kristo. Paulo alisema, “Lakini mimi, hasha,nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo.” Hebu. wote, kutokea wale walio juu kabisa, hadi wale walio chini. kabisa, waelewe kile kinachomaanishwa na kuona fahari juu ya msalaba wa Kristo. Msalaba huo yapasa ubebwe kiume na kwa ujasiri. Kristo alisema, “Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.” Na kwa wale wote watakaouinua na kuuchukua kama Kristo, msalaba ni ishara ya taji ya utukufu ambayo itadumu milele....
             Hii ni sayansi ya juu sana kuliko zote tunazoweza kujifunza, --sayansi ya wokovu. Msalaba wa Kalvari, ukitazamwa kwa usabihi,ni falsafa ya kweli na dini safi, isiyo na taka. Ni uzima wa milele kwa wote wanaoamini. Kwa jitihada sana, mstari baada ya mstari, kanuni juu ya kanuni huku kidogo na huku kidogo, yapasa viwekwe na kukaa akilini... Kwamba msalaba wa Kristo una manufaa sasa kama ulivyokuwa wakati wa Paulo na yapasa wauelewe kikamilifu kama ilivyokuwa kwa mtume huyu wa muhimu....
                  Jua kwamba kitu pekee unachoweza kuwa salama kujionea fahari ni kile
kitakachokufungulia malango ya jiji la Mungu. Jifunze kutoka katika Neno la Mungu namna ya kujenga tabia zifaazo ile nchi unayoitafuta. Jua kwamba yapasa mumweke Kristo mbele yenu na kwamba yote yaliyopotea kupitia kwa Adamu, msalaba wa Kristo unarejesha kikamilifu kwa kila roho inayoamini.











Maoni

  1. Nitakuwa nikiwaletea Kesha la Asubuhi kila week wapendwa ikiimbatana na lesson yenye mafungu ya biblia moja kwa moja,auhitajiki kufanya rejea kwenye Biblia mara kwa mara unaposoma biblia

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Somo 8:Yesu Alionesha Huruma Agosti 13-19,2016

TUNAWEZAJE KUITAMBUA IMANI YA KWELI KATIKATI YA DINI NA MADHEHEBU MENGI SANA ULIMWENGUNI LEO?